Mapema leo, nilijumuika na viongozi wa matabaka mbali mbali, mashirika ya kijamii, washika dau kutoka serikali ya kitaifa na Wakazi wa Ndugumnani, Wadi wa Sokoke, eneo bunge la Ganze kuadhimisha siku ya Mazingira duniani katika shule ya msingi ya Ndugumnani.
Kauli mbiu ya siku ya mazingira duniani mwaka huu, “Ardhi Yetu, Mustakabali Wetu, Sisi ni #Urejesho wa Kizazi,” imeangazia kwa kina changamoto, fursa na vile vile wajibu wetu wa pamoja katika utunzaji wa mazingira na ardhi yetu ambayo ni rasilimali yetu kubwa na msingi wa maisha yetu ya sasa na baadaye.
Kupitia Idara yetu ya Mazingira, tumezindua mradi wa Kijani wa Kilifi, unaolenga kupanda zaidi ya miti milioni moja katika kaunti nzima ambao tutahifadhi mazingira yetu na kutoa ajira za kazi kwa vijana wetu. Juhudi zetu katika kujenga mifumo ya uvunaji na kuhifadhi maji pia zimeongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wetu wa kustahimili ukame, na kuhakikisha kuwa jamii zetu zinapata maji hata nyakati za ukame.
Serikali ya Kaunti vile vile inaendelea na mipango ya uboreshaji wa huduma katika sekta zetu za afya, elimu, maji, haswa katika Wadi ya Sokoke, eneo bunge zima la Ganze na Kilifi kwa jumla. Tuzidi kushirikiana katika ustawishaji wa Kaunti yetu.